UZALISHAJI WA VITUNGUU KIBIASHARA – LIMA KIJANJA (SMART FARMING)

UZALISHAJI WA VITUNGUU KIBIASHARA – LIMA KIJANJA (SMART FARMING)

Habari rafiki, Natumaini unaendelea vyema kabisa na harakati za kusaka mafanikio kupitia kilimo. Nitumie fursaa hii kukukaribisha sana kwenye blog hii ya kilimo (www.kilimo.net), kupitia blog hii utajifunza kila kitu ukatachotaka kuhusu kilimo na biashara ya mazao ya kilimo. Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha unafanikiwa kwenye kilimo. Leo tunakwenda kuanza  kujifunza kwa kina kuhusu kilimo cha Vitunguu. Karibu sana.


Utangulizi
Vitunguu maji kwa kitaalamu hujulikana kama Allium cepana kwa kiingereza huitwa Bulb Onions. Vitunguu ni zao muhimu sana sio kwa matumizi ya ndani tu lakini pia ni zao la kibiashara linaloweza kukuletea kipato kikubwa.  Vitunguu ni zao la bustani ambalo lipo kwenye kundi la mboga (vegetables). Zao hili ni maarufu kutokana na thamani ya virutubisho ilivyonavyo na ladha yake kwenye mapishi ya vyakula mbalimbali.
 
ASILI YA VITUNGUU
Vitunguu vinaaminika, vilianzia Uturuki (Turkey) japo maandiko mengine yanajumuisha pia, Iran, Afghanistan, Pakistan na Kaskazini mwa China kama ndio asili ya vitunguu maji.
 
Uzalishaji wa Vitungu Duniani
China ndiyo inaongoza kwa uzalishaji wa vitunguu vingi duniani, ikifuatiwa na India kisha Marekani. Kwa Afrika Nchi zinaoongoza kwa uzalishaji wa Vitunguu ni Misri, Algeria, Morocco, Nigeria, Afrika Kusini na Niger. Kwa Africa Mashariki Tanzania ndiyo inayoongoza ififuatiwa na Kenya.
 Kwa uzalishaji wenye tija Korea ndiyo inayoongoza, ikifuatiwa na marekani kisha Uhispania (Spain). Katika uzalishaji wenye tija kubwa (high productivity) tunamaanisha wingi wa mavuno kwa eneo (ekari au hekta). Korea wao wanavuna Tani 26.8 kwa ekari (sawa na Tani 67 kwa hekta) kwa vipimo vya magunia ni sawa na magunia 223 kwa ekari moja. Marekani wanavuna tani 22.8  kwa ekari (sawa na tani 57 kwa hekta), kwa vipimo vya magunia ni sawa na magunia 190 kwa ekari. Uhispania wao wanavuna magunia 180 kwa ekari.
 
Uzalishaji wa Vitunguu kwa Tanzania
Kwa Tanzania vitunguu huzalishwa katik maeneo na hali ya hewa mbalimbali, lakini kwa wingi  vitunguu huzalishwa Arusha (Karatu – Mang’ola), Singida, Iringa, Morogoro na Dodoma.
Hapa nchini vitunguu hulimwa kipindi chote cha mwaka kutegemeana na eneo, lakini uzalishaji mkubwa au msimu mkubwa wa vitunguu huonekana kati ya mwezi July na September (mwezi wa 7 hadi wa 9), Hivyo mara nyingi miezi hiyo Vitunguu hua na bei ndogo maana uzalishaji ni mkubwa. Msimu mdogo (low season) wa Vitunguu kwa Tanzania ni kati ya Mwezi wa Kwanza hadi wa Nne (January hadi April).Kipindi hichi maeneo mengi hua na Mvua nyingi ambayo kwa kwawaida huathiri kilimo cha Vitunguu, hii hupelekea wazalishaji wachache kumudu kuzalisha vitunguu. Hii pia huchangiwa na gharama kubwa za uzalishaji kipindi cha mvua, na mavuno yake hua kidogo kulinganisha na msimu wa kiangazi. Kipindi hichi mara nyingi bei ya Vitunguu hua juu zaidi.
 
AINA ZA VITUNGUU
Vitunguu maji vimegawanyika katika makundi matatu:
 
Kundi la Kwanza: Vitunguu vyeupe (White Onions). Vitunguu hivi ni vyeupe nje na nadni pia: Mfano ni White granex, snow white
 
 
Kundi La Pili: Vitunguu vya Njano (Yellow Onions). Vitunguu hivi hua na rangi ya dhahabu kwa nje, ila ndani nyama yake ni ya njano mpauko.  Vitunguu hivi ni vitamu (ladha ya sukari) kuliko aina nyingine ya vitunguu. Mfano: Texas Supersweet, Walla Walla Sweet, Granex Yellow Hybrid, Candy Hybrid
 
Kundi la Tatu: Vitunguu vyekundu (Red Onions): Hivi vina rangi nyekundu kwa nje na ndani kunakua na rangi nyeupe. Mfano  Red Creole, Red Bombay, Neptune F1, Tajirika, Meru Super, Mang’ola Red, JAMBAR F1, n.k  
 
Aina hizi za vitunguu vyekundu ndizo hupendwa zaidi na walaji na ndio huzalishwa kwa wingi. Hivyo katika mafunzo yetu tutajikita zaidi kwenye aina hizi za vitunguu vyekundu. 
 


AINA ZA MBEGU ZA VITUNGUU

Kuna aina tatu za mbegu za vitunguu.
Aina ya Kwanza: Mbegu za Kienyeji:  Hizi ni zile mbegu zinazozalishwa na wakulima wenyewe. Mara nyingi mbegu hizi zinakua hazijathibitishwa na wataalamu kutoka taasisi ya kuthibiti ubora wa mbegu (TOSCI). Wakulima wanazalisha mbegu hizi na kuwauzia wakulima wengine kwa kutumia kipimo cha kilo au debe. Wakulima wengi hupendelea mbegu hizi za kienyeji kwa vile bei yake ni ndogo. Mbegu hizi maeneo mengi huuzwa kati ya 20,000 hadi 30,000 kwa Kilo moja ya mebgu.  Kutokana na kwamba mbegu hizi zina ubora mdogo, mkulima inambidi atumie mbegu nyingi ili kutosheleza mahitaji ya ekari moja. Kwa ekari moja mkulima hutumia kilo 6 hadi 10 za mbegu hizi ili kutosheleza. Kama mtaalamu wa kilimo simshauri mkulima anayetaka kulima kibiashara kutumia mbegu hizi za kienyeji kwa maana hata Mavuno yake hayatabiriki.
Ila Sio kwamba mbegu zote zinazozalishwa na wakulima ni mbaya, hapana. Upo utaratibu wa wakulima kuzalisha mbegu kitaalamu kwa kufuata utaratibu ulipo kisheria. Mbegu hizo zinazozalishwa na wakulima kitaalamu huitwa mbegu za daraja la kuazimiwa (quality declared seeds) au kwa kifupi huitwa QDS. Mbegu hizi za QDS zina mipaka yake ya eneo la kutumika. Na wazalishaji wa QDS lazima wapate mafunzo na wasajiliwe na Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu (Tanzania Official Seed Certification Institute) au kwa kifupi TOSCI. TOSCI pia wana utaratibu wa kufanya ukaguzi na kutoa kibali cha mbegu hizo za QDS kuuzwa kama zimekizi vigezo husika. Kama hazijakizi mbegu hizo haziruhusiwi kuuzwa kwa wakulima.
 
Aina ya Pili:  Mbegu za Kawaida (Open Pollinated Varieties) au kwa kifupi huitwa OPV. Mbegu hizi zimezalishwa kitaalamu kwa njia ya Uchavushaji ya wazi (Open Pollination). Mbegu hizi ndio zinazouzwa kwa wingi na makampuni ya mbegu.  Bei yake ni kati ya 60,000 hadi 100,000 kwa kilo. Hii inategemeana na kampuni na aina ya mbegu. Mbegu hizi kwa ekari moja utatumia Kilo 3 hadi 4. Mfano wa mbegu za OPV ni: Bombay Red, Red Creole, Tajirika, Meru Super n.k.
 
Aina ya Tatu: Mbegu Chotara (Hybrid): Hizi ni aina ya mbegu zinazozalishwa kitaalamu sana kuliko hizo aina nyingine nilizozitaja hapo juu. Mbegu hizi hua na sifa za kipekee, kama vile kua na mavuno mengi, kuwa na ukinzani kwa baadhi ya magonjwa, kukomaa haraka n.k. Nyingine hutengenezwa kutokana na sifa maalumu zinazohitajika na walaji au soko, kama vile rangi, ukubwa (size), harufu, ladha n.k. Pia mbegu hizi huuzwa ghali zaidi. Bei yake ni kati ya 300,000 hadi 600,000 kwa Kilo moja. Kilo moja na nusu au Kilo 2 hutosha kwa ekari moja.   Mfano wa mbegu hizi ni kama Neptune F1, RedStar F1, JAMBAR F1 n.k
 
Mahitaji ya Kiikolojia kwa ajili ya uzalishaji wa Vitunguu (Ecological requirements)
Hali ya Hewa: Vitunguu hustawi maeneo ambayo hayana mvua nyingi, yenye baridi kiasi, wakati wa joto na yasiyo na joto kali.
Udongo:Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha.  Udongo ambao ni mlaini usioshikamana (loose soil) wenye kuruhusu mizizi kupenya kirahisi, unaohifadhi unyevunyevu kama mfinyanzi tifutifu. Udongo unaotuamisha maji haufai.
 
Maandalizi ya shamba la Vitunguu:
Lima shamba lako vizuri, angalau utifue/ufukue udongo kwa kina cha sentimita 15 kwenda chini. Shamba lako lilimwe wiki 2 au 3 kabla ya upandaji wa vitunguu.
Lainisha udongo au kwa kitaalamu inaitwa Harrowing. Yaani yale mabonge makubwa makubwa ya udongo yanagongwa na kutengneza udongo mlaini. Harrow ifanyike wiki 2 au 3  baada ya kulima. Zipo trekta zinazofungwa mashine ya kufanya harrowing.
Tengeneza matuta au vitalu kwa ajili ya kupandia. Kwa matokeo mazuri matuta ya vitunguu yawe yale ya kuinuka (raised bed) angalu mwinuko wenye urefu wa sentimita 20. Upana wa tuta uwe mita moja.
 
 
Upandaji wa Vitunguu: Vitunguu vinaweza kupandwa kwa njia mbili:

 Njia ya kwanza:  Upandaji wa moja kwa moja (direct planting).
Namna ya Kupanda vitunguu kwa njia ya moja kwa moja:
Andaa shamba vizuri, udongo uwe mlaini, usiwe na mabongemabonge ya udongo. Weka  mbolea ya samadi kwa kutawanya (broadcasting) kisha ichanganye vizuri na udongo. Mbolea ya samadi inayotosha kwa ekari moja ni tani 16.
Baada ya kuchanganya vizuri samadi kwenye udongo, tengeneza mistari (drills) yenye kina cha sentimita 2.5 na yenye umbali wa sentimita 30 kutoka mstari hadi mstari. Kumbuka hii mistari ni kama mifereji midogo mwembamba ambayo itatumika kuweka mbegu. Hivyo zingatia vipimo.
Weka mbolea ya kupandia kwenye hiyo mistari uliyotengeneza. Mbolea hii inapaswa kua na kirutubisho cha Phosphorous (Phosphate fertilizer). Mfano wa mbolea za kupandia ni kama DAP, MAP, TSP n.k. Ukishanyunyizia mbolea ya kupandia ichanganye vizuri na udongo.
Sia mbegu kwenye hiyo mifereji halafu funika kwa udongo. Kisha mwagilia mara kwa mara kadri mahitaji yanavyoongezeka. Hapa ina maana kwamba kadri mmea unavyokua ndivyo unahitaji maji mengi zaidi.
Mimea ikashakua, punguza mimea, na uache sentimita 8 (cm) kati ya mmea na mmea. Ile mimea unayoipunguza kwa kuing’oa inaweza kupandwa sehemu nyingine.
Hivyo basi nafasi ya mimea itakua ni 30 X 8 cm. Yaani mstari hadi mstari ni sentimita 30 na nafasi ya mche hadi mche ni sentimita 8.
 
Njia ya pili: Upandikizaji wa miche (transplanting). Hapa Miche inakuzwa kwenye kitalu kwa wiki 6 hadi 8 tangu kisia mbegu kisha inahamishiwa shambani. Inakadiriwa kwamba wiki 6 hadi 8 miche itakua imefikia kiwango kizuri cha ukuaji kwa ajili ya kuhamishiwa kwenye shamba kuu (main field). Hii ndio njia inayoshauriwa zaidi na ndiyo inayotumia na wakulima wengi wa vitunguu.
 
Jinsi ya Kukuza Miche Vitunguu kwenye Kitalu
Tengeneza matuta yaliyoinuka (raised seed beds) yenye upana wa mita 1 na urefu utakaopenda. Urefu mzuri wa tuta unaweza kuanzia mita 2 hadi 5. Idadi ya matututa itategemea na wingi wa mbegu unazotaka kusia.
Weka Mbolea ya samadi iliyooza vizuri. Itawanye vizuri kwenye matuta ya kitalu
Weka Mbolea ya kupandia ya viwandani kama TSP au MAP. Kisha changanya vizuri na udongo. Hakikisha Samadi, mbolea ya ya Kupandia TSP vyote vinachanganyika vizuri kwenye udongo.
Tengeneza mistari ambayo iko kama mifereji midogo yenye urefu wa sentimita 2. Mistari hiyo iwe umbali wa sentimita 5 kutoka mstari hadi mstari.
Sia mbegu za vitunguu kwenye mistari hiyo kisha funika na udongo kidogo.
Funika tuta lako kwa nyasi zilizokauka. Nyasi zinasaidia kutunza unyevunyevu wa udongo pamoja na joto la udongo litakalosaidia miche kuota vizuri.
 
Mwagilia maji mara kwa mara. Umwagiliaji unapaswa kuzingatia unyevunyevu wa udongo. Epuka kuzidisha maji kwenye kitalu maana husababisha magonjwa ya fungus (fungal diseases) kama Kinyausi (Damping Off).
Ondoa Nyasi mara mimea inapoanza kuchomoza juu ya udongo. Kama ni msimu wa jua kali, tengeneza kichanja ambacho juu yake utafunika na nyasi chache ili kupunguza ukali wa mionzi ya jua kwenye miche. Kila tuta unaweza kulijengea kichanja chake.
 
Ng’o magugu kwenye kitalu. Hakikisha kitalu hakina magugu wakati wote, kwa maana vitunguu vina mizizi mifupi (shallow roots) na haiwezi  kushindana na magugu.
Pandikiza miche yako kwenye shamba kuu mara miche inapofikia urefu wa sentimita 15. Mara nyingi huchukua muda wa wiki 6 hadi 8 toka kusia mbegu hadi kufikia kupandikizwa. Maeneo ya joto ukuaji wa miche ni wa haraka zaidi, chini ya wiki 6 miche inakua tayari.
 
Upandikizaji wa Vitunguu.
Vitunguu vinapsawa kupandikizwa wakati wa asubuhi au au jioni. Wakati wa jioni ndio mzuri zaidi wa kuhapandikiza miche.
Miche inapaswa kupandwa kina kilekile kama ilivyokua kwenye kitalu. Yaani mche unapong’olewa kwenye kitalu kuna sehemu ilikua chini ya ardhi. Kwenye kupandikiza urefu uleule uliokua chini ya ardhi wakati mche ulipokua kwenye kitalu ndio unapaswa kufunikwa na udongo wakati wa kupandikiza.
Nafasi ya upandaji wa miche unapaswa kua sentimita 30 kwa 8 (30 X8 cm). Yaani urefu wa mstari na mstari uwe sentimita 30 na nafasi ya mche na mche iwe sentimita 8. Nafasi inaweza kutoafutiana kidogo kulingana na aina ya mbegu, lakini pia kulingana na ukubwa wa kitunguu unachotaka. Ukitaka vitunguu vikubwa, nafasi inaongezeka, yaani vinapandwa mbalimbali. Ukitaka vitunguu vidogo unapunguza nafasi, yaani unapanda karibukaribu.
 

 
Uwekaji wa Mbolea: Kwenye zao la Vitunguu, kuna makundi makuu matatu ya mbolea:
Kundi la kwanza: Mbolea za Kupnadia. Hizi huwekwa kabla au mara tu ya kuhamishia miche shambani. Mbolea hizi zina lengo la kusaidia ukuaji mzuri wa mifumo ya mzizi (root systems) itakayosaidia mmea kufyonza virutubisho na maji kutoka ardhini. Mbolea hizi zina kirutubisho kikuu cha Phosphorous, na huitwa mbolea za fosfeti (Phosphate Fertilizers), kundi hili lina mbolea kama MAP, TSP, DAP, Minjingu n.k
Kundi la Pili: Mbolea za Kukuzia: Mbolea hizi huwekwa kipindi cha ukuaji wa mmea (vegetative growth) na hua na lengo la kuupa mmea ukuaji mzuri utakaopelekea kua na majani mazuri yatakayotengeneza chakula cha kutosha cha kwenye mmea. Kitendo hichi cha mmea kutengeneza chakula chake huitwa Photosynthesis na hufanyikia kwenye majani. Kirutubisho kikuu katika kundi hili la mbolea ni Nitrogen (N). Baadhi ya mbolea zilizopo kwenye kundi hili ni pamoja na UREA, SA, CAN n.k Pia kwenye kundi hili zipo mbolea za maji zinazopigwa kwenye majani (foliar fertilizers) hujulikana pia kama booster.
Kundi la Tatu: Mbolea za Kuzalisha/kukomazia kitungu.Hizi ni zile zinazowekwa kuusaidia  mmea kutengeneza kitunguu (bulb formation).  Kirutubisho kikuu hapa ni Potassium. Ili Kituunguu kiweze kujijenga vizuri na kua na ubora mzuri kinahitaji mbolea zenye kitutubisho cha Potassium. Mfano wa mbolea zenye virutubisho hichi ni Multi K, MOP (Muriate of Potash) n.k
 

Hayo ndio makundi makuu ya mbolea, japokua mbolea hizo hujumuisha pia virutubisho vidogo (micro nutrients) ambavyo vinahitajika kwa udogo kwenye mimea, japokua zina kazi muhimu kwenye mimea.
 
Kwa mpngilio sahihi wa mbolea usisite kuwasiliana nasi.
 

Palizi
Mmea wa kitunguu una mizizi mifupi, hii husababisha kutunguu kuathirika sana na ushindani na magugu. Mizizi mifupi ina maana huufanya kukosa uwezo wa kustahimili ushindani wa magugu. Magugu yana uwezo mkubwa wa kufyonza virutubisho ardhini kuliko mimea ya mazao, na ndio maana magugu hukua kwa haraka kuliko mazao.  Hivyo inashauriwa katika shamba la vitunguu hakikisha unafanya palizi kwa wakati. Idadi ya palizi inategemea na aina na wingi wa magugu wa eneo husika. Kwenye ameneo yenye magugu mengi, palizi hufika hadi 4, na kwa maeneo ambapo magugu sio tatizo palizi mbili zinatosha. Kuna mbinu mbalimbali za kfuanya palizi kama matumizi ya dawa za kudhibiti magugu (herbicides), palizi ya mkono (hand weeding) na uwekaji wa matandazo (mulching).
Kwa ushauri wa aina nzuri ya madawa wasiliana nasi.
 

 
Uvunaji wa Vitunguu
Muda wa ukomaaji wa vitungu hutegemea aina ya vitunguu pamoja na hali ya hewa ya eneo husika. Aina za chotora  (hybrid) mara nyingi hukomaa mapema, huchukua miezi 3 hadi 5 baada ya kusia mbegu.  Aina za kawaida (OPV) na zile za kienyeji hazina ukomaaji unaofanana (do not mature uniformly), hukomaa kwa makundi makundi. Pia mara nyingi hukomaa miezi 4 na kuendelea kuanzia kusia mbegu.
Kama shamba lako unatumia umwagiliaji, basi umwagiliaji unapaswa kukoma siku 7 hadi 10 kabla ya kuvuna. Uvunaji unaanza pale majani ya vitunguu yanapoanza kukauka, kupoteza rangi na kujikunja. Yale majani ya nje yanayofunika kitunguu unene wake unapungua. Hizo ndio dalili za kitunguu kua tayari kwa kuvunwa.  Uvunaji wa mapema (early harvest) hupelekea vitunguu ambavyo havijakomaa vizuri, hivyo kusababisha kupoteza maji na  kusinyaa kwa vitunguu wakati wa ukaushaji wa vitunguu. Pia uvunaji wa kuchelewa (late harvest) husabisha kitunguu kupoteza rangi yake, kuoza kwa yale maganda/majani yanayokua yamekifunika kitunguu chenyewe (onion bulb). Hivyo basi kitunguu kinapaswa kuvunwa kwa wakati sahihi ili kuepuka hasara inayoweza kutokana na kuwahi au kuchelewa katika uvunaji.
Wakati wa uvunaji, vitunguu hung’olewa toka ardhini, kisha kukatwa mizizi yake ili kuzuia ukuaji wa majani. Baada ya hapo ukaushaji wa vitunguu unaanza.
 
Ukaushaji wa Vitunguu.
Baada ya kuvuna kitunguu, hatua inayofuata ni ukaushaji (curing) na hii inafanyikia palepale shambani. Kukausha kitunguu ni ule mchakato wa kukausha ile shingo ya kitunguu. Shingo ya kitunguu inapokauka inakifunga kitunguu, pia inaziba njia ambazo zinaweza kutumiwa na vijidudu kuingia ndani kuharibu kitungu. Ukaushaji pia husaidia kupata kitunguu chenye ngozi iliyokauka na yenye rangi nzuri. Ngozi tunamaanisha lile ganda la nje lililofunika kitunguu.  Baada ya kung’oa vitunguu shambani unavikusanya kwenye makundi makundi, kisha hayo makundi ya vitunguu unayafunika na majani makavu ili kuepuka kuchomkea na jua na kutengeneza mabaka ya kuchomwa na jua (Sunscald). Muunguzo wa jua (sunscald) yaani kitunguu kinapopigwa na mionzi ya jua huua au huharibu lile ganda la nje na hivyo kupelekea kitunguu muundo usiofaa au kuvutia vijidudu vyenye kusababisha kitunguu kuoza. Viache vitunguu kwa muda wa wiki moja au mbili ili vikauke vizuri, kisha vipakie kwenye magunia kwa ajili ya kwenda kuhifahi au kwa ajili kupeleka sokoni.
 
Uhifadhi wa Vitunguu (Storage)
Kitungu ndio zao lenye uwezo wa kuhifadhika kwa muda mrefu zaidi kuliko mazao yote ya mboga. Kitunguu baada ya kuvunwa bado kinakua ni kiumbe kinachoishi (living organism) ikimaanisha kinaenelea na michakato kama kupumua, kupoteza maji n.k Hivyo uhifadhi wake unahitaji umakini ili kuweza kukaa muda mrefu bila kuharibika. Hii ni tofauti na mazao kama mahindi, maharage n.k, ambapo yakishakaushwa yanabaki na asimilia ndogo sana ya unyevunyevu, na unaweza kuyaweka kwenye pia au dramu na ukafunika na kuziba kabisa  bila kua na hata hewa, na mahidni yakaendelea kukaa salama kabisa. Ila kitunguu ni tofauti, kikikosa hewa kinaharibika. Mbinu na mifumo mizuri ya uhifahi wa kitunguu ni muhimu sana kwa maisha ya vitunguu.
 Jifunze Uvunaji wa Vitunguu kupitia Video. Bonyeza hapa: http://wp.me/p8tHEo-az

 
Bei ya Vitunguu:
Kwa mujibu wa TAHA, Leo tarehe 7.11.2016 Bei ya Kitunguu kwenye masoko mbalimbali ni kama ifuatavyo:

Kariakoo: 100,000TSh./Gunia120Kg
Lushoto: 92,000TSh./Gunia100Kg
Kirumba: 110,000TSh./Gunia100Kg
Arusha: 70,000TSh./Gunia100Kg
Makambako: 70,000TSh./Gunia120Kg
Morogoro: 90,000TSh./Gunia100Kg
Soweto: 83,000TSh./Gunia120Kg
Mwanjelwa: 146,000TSh./Gunia120Kg
Mwanakwerekwe ZnZ: 110,000TSh./Gunia120Kg
Dodoma: 70,000TSh./Gunia100Kg
Mombasa ZnZ: 100,000TSh./Gunia120Kg
Kongowea Kenya: 103,200TSh./Gunia100Kg
Kawangware Kenya: 100,000TSh./Gunia120Kg
 

Asante sana. Kwa leo tuishie hapo.

Makala ijayo tutaangazia magonjwa na wadudu waharibifu kwa zao la vitunguu na namna ya kuwadhibiti kikamilifu.
Mwandishi wa Makala hii ni Ni mimi Mtaalamu wako wa Kilimo Biashara Daudi Mwakalinga. Kwa ushauri au maulizo waweza kuwasiliana nasi kupitia namba ya simu 0763 071007, au waweza kutuandikia email kupitia: ushauri@kilimo.net
 
 
Huduma za Kilimo Biashara
Je ungependa kufahamu gharama zinazohitaji kwenye kilimo cha vitunguu na namna unavyoweza kujua makadirio ya faida utakayoipata?
Je Ungependa kulima Kilimo cha Uhakika Cha Vitunguu? Hata kama huna elimu ya Kilimo?
Je unatamani Kulima vitunguu au zao lolote ila hujui uanzie wapi?
Watu wengi hua wanasikia stori za namna ya kupata faida kubwa kwenye kilimo, lakini wakiingia wanajikuta hawapati matokeo sawa na walivyosikia zile stori/hadhithi. Na wakati mwingine wanapata hasara kabisa. Je unajua kwanini?
Kujua hayo na mengine mengi, usisite kuwasiliana nasi kupitia mawasiliano hayo hapo juu.
 
Kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo hapo juu: Kilimo biashara inakuletea huduma zifuatazo:
Huduma ya Kwanza: Uchambuzi wa Gharama na Faida (Cost benefit Analysis – CBA)  wa Zao lolote utakalotaka kulima Kibiashara.
Kwanini CBA? Baadhi ya Manufaa ya kuanza na CBA ni:
CBA itakusaidia kujua Rasilimali na gharama zinazohitajika kwenye uwekezaji wa kilimo unachotaka kufanya. Hii itakusaidia kufanya maamuzi ya kuendelea na wazo la kulima zao hilo au itakubidi ufanye zao lingine.
CBA itakusaidia kujua mgawanyiko wa gharama zinazohitajika. Mfano kama kilimo cha vitunguu kinahitaji mtaji wa milioni 2. Haina maana kwamba lazima uwe na hizo milioni mbili ndio uanze kilimo cha Vitunguu. Inaweza kua inahitajika laki 5, halafu baada ya mwezi ikahitajika milioni moja, halafu mwishowe ikahitajika laki 5. Sasa bila kujua mgawanyiko huo unaweza kudhani ni ngumu kufanya kilimo cha vitunguu kwasababu ya mtaji mkubwa unaohitajika, kumbe unaweza kuanza na kiasi fulani. CBA itakupa picha kamili kwenye hilo.
CBA itakusaidia kujua makadirio ya mavuno na mapato yatakayotokana na Kilimo cha zao unalotaka kufanya. Hakuna mtu anayependa kufanya kitu bila kujua manufaa ya kile anachokifanya. Hivyo CBA itakupa picha ya kile utakachokipata.
Huduma hii inapatikana kwa gharama ndogo ya 20,000/= (Elfu Ishirini tu).
 
Huduma ya Pili: Master Plan. Huu ni Muongozo au Mpango kazi wa Kilimo cha zao unalotaka kulima kibiashara. Mpangilio huu unakuonyesha shughuli zote za Shambani na muda wake wa kufanyika. Hii itawasaidia wale ambao wanataka kufanya kilimo lakini hawajui kipi kianze na kipi kifuate. Muongozo huu utakuonyesha aina ya mbolea na kiasi kinachohitajika, aina za madawa ya magonjwa na wadudu na kiasi gani cha uchanganyaji wa dawa hizo, Umwagiliaji,  na mambo mengine mengi.
Gharama ya kutengnenezewa Mungozo (Master Plan) ni 20,000/= (Elfu Ishirini tu).
 
Kwa watakaohitaji Huduma zote mbili watafanyiwa kwa 30,000/= (Elfu thelathini tu)
 

Kupata huduma hizi na nyingine nyingi waweza kuwasiliana nasi kupitia namba ya simu 0763 071007, au waweza kutuandikia email kupitia: ushauri@kilimo.net

www.kilimo.net 

Response to "UZALISHAJI WA VITUNGUU KIBIASHARA – LIMA KIJANJA (SMART FARMING)"

  • Ahsante sana mtaalam, makala inaeleweka vizuri sana. Umeeleza vizuri sana kwenye mbolea zinazohitajika lkn umesahau kitu muhimu sana: kiasi gani kwa hekta au eka? Ni kiasi gani cha mbolea ya kupandia, ya kukuzia, na MOP kinahitajika?

  • Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *