Haya Ndio Mapinduzi Makubwa Tunayohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Kilimo.

Haya Ndio Mapinduzi Makubwa Tunayohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Kilimo.

Sekta ya kilimo ndio sekta inayoajri watu wengi kwa hapa Tanznia inakaridiriwa zaidi ya aslimia 80 ya watanznaia wanategemea sekta hii aidha moja kwa moja au wananufaika kwa namna moja au nyingine. Kwa ujumla hakuna nchi yeyote duniani amabyo iliendelea bila kuwekeza kwenye kilimo, basi kama ipo zitakua ni chache sana. Hata hizo nchi zenye viwanda vikubwa malighafi zake zinatokana na kilimo. Hii inaonyesha kwamba bila kilimo uchumi wa nchi utakua mashakani. Tofauti ya nchi tajiri na nchi masikini(kama zinavyoitwa nchi zinazoendelea) ni kwamba kwa nchi tajiri kilimo ni uwekezaji unatiliwa umuhimu mkubwa sana. Ndio maana huko matajiri ndio wanaolima lakini kwetu kilimo kimechukuliwa ni cha watu masikini. Na ndio maana ukiwa unalima unaonekana kuwa wewe ni mtu wa kaliba ya chini au uliyeshindwa maisha. Mfano unawezakuta watu mjini wakitoa kauli zinazoonyesha kilimo ni kama chaguo la mwisho. Mara kadhaa utasikia watu wakisema kama mjini pamekushinda rudi kijijini ukalime. Hapa wakimaanisha kilimo ni kama shughuli za ya kishamba na ndio chaguo la mwisho ukishashindwa kila kitu.


Kwa bahati mbaya sio mjini tu ndiko wanakodharau kilimo hata kijijini kwenyewe wapo watu wengi wanaona kilimo ni kama adhabu fulani. Nakumbuka nikiwa kijijini kwetu baada kumaliza kidato cha sita na kupata nafasi ya kwenda kusoma kilimo Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Morogoro baadhi ya ndugu waliumia sana kusikia kwamba naenda kusomea kilimo tena chuo kikuu. Ndugu mmoja alidiriki kuniambia mwanangu naona umepoteza dira yaani unaenda kusomea kilimo chuo kikuu, sasa kweli huko kuna hela? si bora ungeenda hata upolisi ambapo unaanza kupata hela mapema na ajira ni uhakika. Yaani huoni wenzako wanasomea uhasibu kozi nyingne zenye hela. Lakini niliamini ipo siku moja watageuza mtazamo walio nao na mimi ndio nitakua chachu ya mageuzi hayo ya fikra.
Hoja ninayoijenga hapa ni kwamba sisi wenyewe ndio tumekua chanzo cha kufanya vibaya kwa kilimo chetu kwa sababu ya fikra potofu tulizonazo juu ya kilimo. Tunasahau kwamba kilimo ni biashara kama zilivyo biashara nyingine. Hivi tunajifunza nini tunapoona makampuni makubwa yanawekeza kwenye kilimo? Mfano mji wa Arusha kuna Makampuni zaidi ya 20 ya wawekezaji wa nje ambao wamewekeza kwenye kilimo cha maua, mboga mboga, matunda na hata nafaka. Hivyo hivyo kwenye mikoa mingne kuna uwekezaji kutoka nje. Wakati sisi tunachukulia kilimo kama jambo la hovyo hovyo wenzetu wanaingiza teknolojia kwenye kilimo. Mfano nimewahi kufanya kwenye kampuni moja inayozalisha mbegu chotara ambayo ipo Arusha ambapo nilikua Meneja Msaidiz kwenye kitengo cha Operesheni na Uzalishaji ambapo wana mwagilia kwa kutumia mfumo wa kompyuta (Computerized Irrigation system). Huhitaji kuwepo ili mashamba yamwagiliwe hata ukiwa haupo una seti mitambo automatiki kazi inaendelea. Pia mimea inawekewa feni za kisasa ili kudhibiti hali ya hewa( joto na unyevunyevu kwenye hewa au humidity) ili kuhakikisha mbegu inakua na ubora wa hali ya juu.
Lakini swali la kujiuliza je walianzia wapi hadi wakafika hapo? Jibu ni kwamba walianzia mbali sana, kampuni yenyewe ina zaidi ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, na ilianzishwa kama kama kampuni ya familia huko nchini Uholanzi mnamo mwaka 1938, mwanzilishi alianza kwa kuuza mbegu za mbogamboga kwa wakulima wenzie, baadaye akaanza kidogokidogo kuzalisha mbegu leo hii ndio kampuni inayoongoza duniani kwa kuzalisha mbegu chotara za mbogamboga. Kwa sasa imesambaa zaidi ya nchi 20 duniani ikiwemo Tanzania na ni kampuni ya mabilioni ya hela. Hivi sasa kampuni inaongozwa na mjukuu yaani aliyeianzisha aliiongoza akamwachia motto wake naye akaiongoza leo hii mjukuu ndiye CEO na bado inakua kwa kasi sana. Japo mwanzilishi alianzia katika hali duni na ya chini sana lakini alikua na maono makubwa na alikua kiipenda kazi yake.
Tunachojifunza hapa ni kwamba hatuhitaji mabilioni ya hela kufika walikofika wenzetu, hayo yote kwa sasa hayatatusaidia. Ndio maana kila mwaka tunatenga mabilioni ya hela lakini kilimo chetu bado hikipigi hatua. Tunasahau kwamba hatuwezi kubadilisha nje wakati ndani bado hatujabadilika. Vijana wengi tunataka pesa za haraka haraka tukiambiwa tuwekeze kwa malengo ya kuanza kupata faida miaka 3 au 5 mbele hakuna nayetaka kusikia hiyo habari. Tunakosa uvumilivu. Angalia hata matajiri wengi wa Tanzania kilimo ndicho kiliwatoa. Baadhi ya watu ambao nimekua nikiwafuatilia ni Bilionea Eric Shigongo. Leo hii tunamwona Shigongo hapo alikofika amefanya sana kilimo, amelima sana mananasi huko pwani na ni biashara iliyokua inamlipa sana. Sasa hivi anawekeza kwenye madini na biashara nyingine kubwa lakini mweynyewe anakiri kilimo ndicho kilimtoa.
Hitimisho: Niseme tu napenda kutambua juhudi za watu ambao wameanza kuamka na kuchukulia kilimo kama uwekezaji unaolipa. Wapo watu amabo wameadhamiria kufanya kitu katika kilimo. Natamani kuona watanzania wengi tukifuata nyayo zao. Lazima tubadili fikra zetu lazima tuwe na mitazamo chanya kuhusu kilimo. Asanteni sana tukutane wiki ijayo katika makala nyingne ya kilimo.

No comments.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *